Tuesday, 12 July 2011

Sungura Apanga Njama


Ikawa basi siku moja, Sungura akawaza jinsi wanyama wala mimea wanavyoweza kujiondoa kwenye minyororo ya utawala wa ki imla wa mfalme Simba na majemedari wake. Akamwendea Pundamilia kuumuliza maoni yake na kumshawishi waungane wamwondoe Simba kutoka kiti chake cha enzi. “Naja kuuliza maoni yako kuhusu huyu mfalme wetu kwani naona hafai kwetu sisi” Sungura akmwambia Pundamilia. “Tazama, huwezi kula nyasi kwa amani kwani kila wakati wajichunga huenda mmoja wa majemedari wa Simba akatokea na kukuua anywe damu yako” akaendelea Sungura. Pundamilia akamsikiliza naye Sungura akazidi kumshawishi “hao majemedari hata hawana nguvu, ukimtandika mmoja teke moja tu la ubavu atakufa tu, lakini kwa sababu ya uoga huwezi” akamalizia hoja yake Sungura.

Baada ya kuwa kimya kwa kipindi, Pundamilia akajibu akasema “nenda zako usiniletee majaribu. Uonavyo ningali hai na sura yangu haijaharibiwa kwa viboko kama ilivyo ya dada yangu Punda muishi na binadamu. Akatulia kidogo akamtazama Sungura kwa macho ya huzuni na kuendelea “katika nchi ya binadamu alikopelekwa mateka, dadangu ndio hubebeshwa mitungi ya maji, ndio hubebeshwa magunia ya mizigo, hutumika kulima, maskini kazi yote hufanyishwa yeye hata nafasi ya kula nyasi kama hii nilayo mimi hapati kabisa”.

Sungura hakufa moyo “hebu fikiria ni akina Pundamilia wangapi wameyapoteza maisha chini ya majemedari wa Mfalme wa Nyika. Sitakushawishi zaidi, lakini nakuomba uyatafakari hayo niliokwambia” Sungura akamwambia kisha akaenda zake.

Sungura alizidi kutafakari sana hayo ya mfalme na jinsi angeondolewa mamlakani. Iwapo kungefanywa sensa ya wanayama pori wote, wale ambao hula mimea ndio waliowengi kuwashinda wale wala nyama. Ni kwa nini basi wale hula nyama ndio wawe wanatawala na kuwahangaisha walio wengi? Utawala huo ungeweza kubadilishwa vipi. Kwa kimo, yeye Sungura alikuwa mdogo tu, lakini akili alikuwa nazo, bali hangeweza kufanya mapindizi akiwa peke yake. Yeye alikuwa tayari kuwa mwanzilishi wa mapinduzi. Alikuwa tayari kutolewa zaka ili wanyama wengine wapate uhuru kutoka kwa utawala wa kimila nyikani.

No comments:

Post a Comment