Tuesday, 12 July 2011

Imla ya Mfalme Simba


Tangu zamani za kale, hamna mnyama yeyote katika nchi ya Pori aliye jaribu hata wakati mmoja kubishana na Simba, wala kuteta naye wala hata kuwaza japo kwa ndoto tu kwamba Simba ang’atuliwa kutoka kwa cheo chake cha enzi kama mfalme wa Nchi ya Pori. Hilo halikupingwa wala halingelipingika. Tangu atawazwe, alitawala kwa nguvu na uwezo wake wote, imla hiyo ya Pori.

Wanyama wengine wa nchi ya Pori waliishi kwa uoga mwingi, wakijaribu wawezavyo kutopitia njia aipitiayo mfalme Simba. Wanyama ambao waliishi na binadamu kama vile Mbwa, Ng’ombe na hata punda walitamani kuishi nyikani kwani kwao waliona kuna amani nyikani. Hasa punda na Mbwa walitamani kuishi maisha ambayo wangeepuka kichapo walichokuwa wapata kutoka kwa binadamu naye Ng’ombe alitamani maziwa yake yabaki kuwa ya ndama wake na wala siyo kutumika na binadamu kulisha watoto wake na yeye mwenyewe. Laiti wangelijua maisha ya woga walioishi wanyama kama vile Punda Milia, Nyati, Swara, Paa na wengineo walio hofia kuuliwa na Simba au majemedari zake.

Mara kwa mara Simba alinguruma na kwa sauti kuu kuwambia wanyama wengine  “tazameni enyi wanyama wa wenzangu wan chi ya Pori jinsi wenzetu wanavyoteseka katika nchi jirani ya binadamu. Punda hufanyishwa kazi ya kitumwa na baadaye huchapwa mijeledi isio kifani. Paka ambaye ni binamu yangu mimi hulishwa mabaki ya chakula lau sivyo kujitafutia chakula kisicho faa kama vile Mapanya na Mapanya-buku. Basi sisi hapa nyikani, tuzoee kuitunza amani yetu na tuwe na heshima kwa viongozi wetu”.

Ama Simba alikuwa mfalme wa ki imla. Alizugukwa na kulindwa na majemedari kama vile Fisi na Chui ambaye alikuwa Jemedari Mkuu. Chakula chao kilikuwa wanyama walao mimea. Kwa sababu hio, Swara, Sungura, Pundamilia, Twiga, na hata Nyati na Faru walimwogopa na kumchukia sana Simba, Fisi, na Chui. Kwa makadirio yao, Simba hakuwa mbaya, bali hao majemedari wake kwani hao ndio walowezi na wachochezi.

No comments:

Post a Comment