Wednesday 13 July 2011

Njama Inaiva Sehemu ya Pili


Hapo Sungura akajitolea kuwakusanya wanyama wote walao mimea na wengine wanao waunga mkono wakutane katika tambarare ilio katikati ya pori ambako kwa mbali wanaweza kuwaona majemedari na watumishi wa mfalme iwapo watavamiwa. Kwenye mkutano huo watawasihi wanyama hao wakatae mamlaka ya Simba wa wanyama pori. Swara akaongeza maoni yake kwamba badala ya Sungura kufanya hio kazi peke yake, wagawanye ili yeye Swara awaambie Ndovu, Nyati and Pundamilia ilhali Sungura akazungumze na Twiga, Ngiri, na pia atume ujumbe kwa viongozi wa nchi jirani ya binadamu na pia kwa nchi za wanyama maji na ndege wa angani. Ujumbe hasa kwa nchi ya binadamu ulikuwa muhimu kwani wakiweza kusaidia mpango huo, ingekuwa rahisi mno kumng’atua Simba mamlakani. Wakakubaliana na wakaenda zao kuanza kazi. Lakini Sungura akawa ana wasiwasi na akarudi tena kwake Swara. “Kuna jambo ndogo ambalo nimelikumbuka” akamwambia Swara. “Ni muhimu tuwekeane ahadi kwamba tutalinda kwa siri kubwa mambo haya ili yasimfikie mfalme kabla ya kuyapanga vizuri. Maoni yangu ni kuwa tule kiapo cha kuweka siri” Lakini Swara hakutaka kula kiapo. Kulingana naye wale swara wengine wote ambao wamekufa mikononi mwa simba na wajakazi wake walikuwa ishara kubwa kuliko kiapo. Fauka ya hayo, nia ya kuwakomboa wenzao ilikuwa na uzito mwingi kuliko kula hicho kiapo. Akasisitiza kuwa kiapo chake yeye ni hio nia ya ukombozi wa wanyama.

No comments:

Post a Comment